FUTARI YA TENDE NA FAIDA ZAKE
Na: Mujahid Mwinyimvua
“Enyi
watu kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate
nyayo za shetani, bila shaka yeye kwenu ni adui dhahiri (Qur‟an: 2:168).
“Enyi Mlioamini kuleni vizuri tulivyokuruzukuni, na Mumshukuru Mwenyezi
Mungu, ikiwa mnamuabudu yeye peke yake”. (Qur‟an: 2:172). “Na kuleni
katika vile alivyokuruzukuni Mwenyezi Mungu vilivyo vizuri na halali na
Mcheni Mwenyezi Mungu ambaye nyinyi mnamwamini (Qur‟an: 5: 88). “......
na kuleni (vizuri) na kunyweni (vizuri). Lakini msipite kiasi tu. Hakika
yeye (Mwenyezi Mungu) hawapendi wapitao kiasi.” (Qur‟an; 7:31).
Jambo
moja kubwa tunalojifunza katika aya za hapo juu ni kuwa lazima tufanye
uchaguzi wa vile tunavyotaka kula. Uchaguzi huo tunapewa vigezo viwili,
cha kwanza ni uhalali (halaalan) na cha pili ni ubora (twayiiban).
Uchaguzi wa vyakula kwa kigezo cha uhalali hikma yake moja ni kuwasaidia
watu katika jamii kuwa katika amani na utulivu wa kweli. Kwa sababu
watu wakizingatia kigezo hicho watakuwa wanachuma kwa misingi ya
uhalali. Yaani dhulma
mbalimbali kama vile wizi, ujambazi, rushwa,
ulaghai, nchi moja kupora rasilimali za nchi ingine, biashara ya
ukahaba, ushoga, usagaji, madawa ya kulevya na kupunja vipimo
hazitakuwepo. Pia, rushwa ya ngono na wizi kama ule wa fedha za EPA,
Richmond, kuingiza samaki wenye sumu, ujanja wa kupandisha bei ya bidhaa
wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani, mambo yote hayo yasingekuwepo.
Kuhusu
uchaguzi kwa kuzingatia kigezo cha pili (ubora), ni muhimu kwa uimara
wa afya ya kiwiliwili. Wasomaji hasa waislamu wakumbuke kuwa ingawa
vyakula vilivyo halali ni ruhusa kuvila, lakini muhimu kujua kuwa ubora
wa hivyo vyakula unatofautiana kama tunavyofahamishwa na Mola wetu
katika aya ifuatayo: ''Na katika ardhi muna vipande vinavyoungana (na
kuzaa kwake namna mbalimbali) na muna mabustani ya mizabibu, na mimea
mingine, na mitende ichipuayo katika shina moja na isiyochipua katika
shina moja. Vyote vinanoshelezwa (vinamiminiwa) na maji yale yale; na
tunavifanya bora baadhi yake (kuliko)
vyengine katika kula.
Hakika katika haya zimo ishara kwa watu wanaotia mambo akilini''. (Raad,
13.3). Kwa kuwa ubora wa vyakula vya mimea inatofautiana, na vyakula
vya nyama na samaki navyo viko tofauti kwa sababu vinategemea vyakula
vinavyotokana na mimea.
Ni dhahiri kuwa watu makini watafanya
uchaguzi wa vyakula kama Mwenyezi Mungu alivyowahimiza. Bahati mbaya ya
mambo kwa watu wengi, wakiwemo waislamu hawajishughulishi kutafuta elimu
ya kujua mambo ya vyakula. Kwa mfano, vyakula vya kukaanga na vile vya
kuchemsha vipi ni hatari kwa afya ya mlaji? Ni kwa namna gani ulaji
mbaya (kama vile mafuta mengi) unasababisha upungufu wa nguvu za kiume
au upungufu wa nguvu za kike. Yaani, watu kushindwa au kuchukia kufanya
jimai kwa mwezi au zaidi hali yakuwa wako katika ndoa. Hili ni tatizo
lilanlokuwa kwa kasi hapa Tanzania, uliza madakrari au soma vitabu au
magazeti utajuwa ukubwa wa tatizo hili. Allah atulinde na hilo janga.
Jambo
lingine tunalojifunza kutokana na aya tulizozinakili awali (2:168,
2:172, 5:88, 7:31) ni kula kwa kiasi, yaani tusifanye israfu. Ni
masikitiko makubwa kwa waislamu wengi kipindi hiki cha mfungo wa
Ramadhani kutumia muda mwingi asubuhi mpaka jioni kuandaa vyakula vingi
kuliko mahitaji. Matokeo yake vyakula hivyo vinatupwa, wakati kuna
baadhi ya binadamu katika duniani hii wanakufa au watoto hudumaa
kutokakana na kukosa chakula. Mtume Muhammad (s.a.w) amehimiza sana watu
wawe wanapima vyakula vyao. Pia, Mtume (s.aw) amefundisha kuwa mtu
akila aligawe tumbo lake sehemu tatu. Sehemu ya kwanza iwe nafasi ya
chakula, ya pili maji, na ya tatu nafasi ya kuweza kupumua (hewa).
Vilevile, Mtume (s.a.w) amesema mtu akila aache hali ya kuwa kidogo
anasikia njaa. Kwa hakika kama tungekuwa tunafanya uchaguzi sahihi wa
vyakula vyetu, kuwa na tania nzuri ya ulaji na kula kwa kiasi kama
Mwenyezi Mungu na Mtume wake walivyotufundisha tunge weza kufikia lengo
la pili la funga ambalo ni
kuimarisha afya ya kiwiliwili. Kuna
watu baada ya funga ya Ramadhani ati uzito wao unaongezeka. Hawa
walikuwa wanakula sana na hivyo, hawakunufaika kiavya na funga.
Baada
ya utangulizi wa hapo juu, sasa tujikite na faida ya kufuturu kwa tende
na tuone namna tende ilivyo msingi wa kuandaa futari (mlo wa futari
unaoliwa baada ya kukata swaum). Kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume Muhammad
(S.A.W), mfungaji anatakiwa afungue kwa tende au maji, halafu aswali
magharibi na baada ya hapo aendelee kula. Na hapa ndipo tunaposema
kukata swaum na kula futari.
Turejea hadithi ifuatayo ili
kuthibitisha hoja yetu ya hapo juu: Anas (r.a) ameeleza kuwa Mtume
(S.A.W.) alikuwa akifungua kwa tende mbichi zilizokomaa (fresh) kabla ya
kuswali (Magharibi), kama hizi hazi kuwepo alifungua kwa tende
zilizowiva na kukauka (mbivu), na kama hizi hazikuwepo alikunywa mafunda
machache ya maji (Tirmidh na Abu Daud). Pia tunaelezwa katika hadithi
nyingine namna
Mtume (S.A.W) na Maswahaba zake walivyokuwa
wanakula tende za kufuturu ni witiri (1, 3, 5, 7, n.k). Zaidi ya hayo,
tukumbuke msisitizo wa Mtume (s.a.w) wa kuwahi kufuturu mara tu muda
unapofika. “Watu wataendelea kuwa katika heri endapo tu watakuwa
wanaharakisha kufuturu (Sahih Bukhari na Sahih Muslim) ”.
Katika
kuingia ndani zaidi ya mada yetu ya leo, vema turejee wito wa Mwenyezi
Mungu alioutoa katika aya tulizozinukuu hapa juu. ''Hebu Mwanadamu na
atazame chakula chake” (80.24). Yaani sisi wanadamu tafakari, tuchunguze
na tutafiti juu ya vyakula tunavyokula. Tukiacha kukitazama chakula
katika muktadha wa Tauhiid, tunaweza kukitazama chakula katika mitazamo
mingine. Mtazamo mmoja unaoendana na mada yetu, ni kukitazama chakula
katika virutubisho (nutrients) vilivyomo ambavyo ndivyo vinarutubisha
mwili wa mwanadamu. Tukumbuke kuwa habari ya tende ni kubwa kuanzia
historia ya zao hilo, nchi zinazolima, Qur‟an inavyosema kuhusu tende,
Bi Mariamu
(mama yake Yesu -A.S-) alivyokula tende wakati
anajifungua, virutubisho vilivyomo ndani ya tende, manufaa ya tende kama
chakula na dawa, na kadhalika. Lakini kwa makala ya leo itoshe tu kwa
kutazama virutubisho (nutrients) vilivyomo ndani ya tende na faida ya
tende kama chakula na dawa ili waislamu wanufaike kiafya na pia yakini
yao juu ya usahihi wa dini yao uongezeke zaidi na wawe na stadi za
kuwaelimisha wasiokuwa waislamu kwa kutumia lugha watakayo ielewa kwa
urahisi (sayansi ya chakula).
Tukumbuke ni ahadi yake Mwenyezi Mungu
aliyoisema katika Qur‟an kuwa atawaonyesha watu ushahidi wa kuwepo
kwake, ukweli wa Uislamu, Mitume yake, Qur‟an, Kiyama na mambo mengine
kwa kutumia mwanadanu mwenyewe na mazingira yanayo mzunguka, zikiwemo
tende. Rejea Qur‟an: „Tutawaonyesha ishara zetu katika upeo wa mbali na
katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je!
Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu
(Surat Fuss'ilat/H'a Mim Sajdah: 41.53).
Kufuturu kwa tende ni
jambo lenye faida kubwa kama alivyohimiza Mtume (s.a.w). Maendeleo ya
sayansi yanatusaidia kuongeza ufahamu wetu unaosema kuwa tende ni
chakula na pia ni tunda lenye dhamani kubwa sana kwa binadamu. Ukweli
huu ni kwa sasabu zifuatazo. Tende ina asilimia 60 mpaka 70 ya sukari
aina ya glucose na fructose. Mtu akila tende aina hii ya sukari
inanyonywa na utumbo na kuunguzwa na seli na hatimae inatoa nguvu kwa
haraka. Kwa mfungaji swaum nguvu hii humpa furaha na akili yake inatuama
kwa haraka. Ndio kusema haifai kufuturu kwa vyakula vigumu kama vile
hindi la kuchoma au ugali. Tende pia ina vitamini aina ya C kiasi cha
gramu 3, na kiasi kidogo cha vitamini B-complex. Tende zikiwa hazijawiva
sana na mbichi (fresh) ndio zina vitamini nyingi zaidi. Aina hii ndiyo
aliyokuwa anaitumia sana Mtume wetu (S.A.W). Vitamini mbali mbali
huwezesha mwili kuwa na kinga ya kupambana na maradhi. Pia baadhi ya
vitamini zinasaidia kuimarisha mbegu za kiume na kuongeza uwezekano wa
kutunga
mimba. Yaani mbegu za kiume zinasafirishwa kwenda katika nyumba ya uzazi kwa msaada wa baadhi ya vitamini.
Vilevili,
tende ina kiasi fulani cha maji (15% au zaidi) inategemea ilivyo
andaliwa. Maji yana kazi kubwa sana mwilini. Baadhi ya kazi hizo ni
kupoza mwili na kuwezesha kazi mbali mbali zinazotaka mazingira ya
umajimaji kufanyika kwa ufanisi. Tende ina protini kiasi cha asilimia
2.5 na madini asilimia 2.1 (Calcium, Phosphorus, Chuma). Protini ni
muhimu kwa ukuaji na ukarabati wa mwili na viungo vilivyo ndani yake.
Madini yanasaidia kulinda mwili. Tende inakiasi kidogo cha mafuta (0.4%)
ili kukidhi haja ya mwili na haina aina mbaya ya mafuta inayoitwa
cholesterol. Mafuta yana kazi nyingi mwilini, zikiwemo kutoa nguvu na
kutengeneza vitu fulani. Cholesterol pia inakazi muhimu katika mwili,
kinacho takiwa mafuta hayo yasiwe mengi. Yakiwa mengi yana sababisha
maradhi kama vile ya moyo, kiharusi (stroke), unene na presha. Zaidi ya
neema hizo alizoumba Allah, tende ina nyuzi nyuzi za kilishe (dietary
fibres)
kiasi cha asilimia 3.9%. Nyuzi nyuzi hizi zinafaida kubwa katika mwili
wa mwanadamu. Kwanza zinanyonya sumu kutoka tumboni na kuitoa nje pamoja
na kinyesi. Pili, zinasaidia mtu kupata choo kikubwa mara kwa mara
hivyo ananusurika na tatizo la kukosa choo na ugonjwa wa kansa ya
utumbo.
Kwa upande wa faida ya tende kama dawa kwa ufupi ni kuwa.
Tende inasaidia kuondoa tatizo la tumbo kuuma. Hii ni kwa sababu tende
inazuia vijidudu vya maradhi kukua ndani ya utumbo na pia inasaidia
kukua kwa bacteria wazuri ndani ya utumbo. Kwa maneno mengine, ndani ya
utumbo kuna weza kuzaliana aina mbili ya vijidudu aina ya bacteria, wale
wazuri na wale wabaya. Hata hivyo, ifahamike kuwa mtu akinywa maji
machafu, yasiyochemshwa au kuwekwa dawa za kuua vijidudu asitegemee kuwa
tende itamsaidia. Tende haitaweza kufanya kazi hiyo, sababu umeipe
mzigo mkubwa. Tende ikitiwa katika maji usiku kucha (saa 12) na isuguwe
ndani ya maji hayo halafu kunywa ni asbabu ya
Allah kukunusuru na
maradhi ya moyo. Wakati huo huli nyama nyekundu (ngo‟mbe, mbuzi,
kondoo, n.k) kwa wingi na unafanya mazowezi ya viungo mpaka unatoka
jasho. Pendelea kula nyama nyeupe kama vile samaki na kuku (sio wa
kisasa). Gazeti la Daily Times la Uingereza la taerehe 12.10.2005,
liliripoti kuwa samaki wanasaidi kurudisha akili za wazee ambao
wanapoteza kumbukumbu. Pia inafahamika kuwa samaki na ndizi ni mlo bora
kwa kujenga akili za watoto. Haya kina mama na kina baba msikose kuandaa
mlo huo kwa watoto wenu.
Zaidi ya hayo, tende inaimarisha nguvu za
kiume na hivyo kuleta maelewano ndani ya familia. Tende kiasi cha
kiganja kimoja ukiziloweka ndani ya maziwa (fresh) ya mbuzi kwa usiku
mmoja (overnight) na halafu zisage tende humo humo ndani ya maziwa (toa
mbegu). Ongeza unga kidogo wa cardamom (uliza maduka ya dawa za kiarabu,
kihindi, n.k) utengeneze na asali kidogo katika mchanganjyiko huo,
nguvu za kiume zitaimarika na mbegu za uzazi zitakuwa na
afya ya
kuchangia mimba kushika kwa idhini yake Mwenyezi Mungu. Si vizuri
kutumia dawa za dukani. Kama huna budi kuzitumia dawa za dukani, lazima
upate maelekezo ya daktari. Tukumbuke siku hizi kuna biashara kubwa ya
dawa za kukuza makalio, mapaja (hips), matiti na viungo vya uzazi vya
kiume/kike. Kwahiyo, bila kupata uashauri kutoka kwa madaktari waaminifu
kuna hatari kubwa ya kupata dawa ambazo zitapoteza kabisa nguvu zako za
kiume au za kike. Muhimu fanya uchaguzi wa vyakula na fanya mazowezi ya
viungo. Pia pata muda wa kupumzika.
Watoto wanaokaribia kuota meno
husumbuliwa na tumbo la kuharisha. Mtengenezee mtoto juisi nzito ya
tende na asali kidogo (changanya), mpe kijiko kimoja mara tatu kwa siku.
Tumbo litapona na meno yatakuwa imara kwa idhini yake Mola wetu. Hata
hivyo, kuhusu tende pia tuzingatie ushauri ufuatao: Tende zina nasa
vumbi na uchafu mwingine. Kwa hiyo, nunua tende safi iliyofungwa vizuri
na kama unawasiwasi nayo ioshe na maji safi kabla ya kuila.
Kwa
kuzingatia manufaa yapatikanayo ndani ya tende ni vizuri kwa kutumia
mlango wa kiasi kuona msingi wa kuandaa mlo wa futari unaofaa. Kwanza
mlo wa futari tunaokula baada ya kukata swaumu na kuswali Magharibi uwe
laini na uandaliwe na vyakula ambavyo ni rahisi kusagwa tumboni. Pili,
vyakula hivyo viwe vitamu, ila visiwe na sukari nyingi sana. Mfano wa
vyakual hivyo ni ndizi zilizoiva na kupikwa, viazi, maharage, mihogo na
vingine mithili ya hivyo. Vyakula vya futari (na vingine) visiwekwe
chumvi nyingi wala mafuta mengi. Kama mafuta watu watumie yanayotokana
na mimea. Mawese, alizeti, ufuta, mahindi ni miongoni mwa mafuta bora
kabisa. Mboga za majani na matunda (au juisi) ni muhimu wakati wa kula
futari. Ikumbukwi juisi bora ni ile ya kuandaliwa bila kuwekwa
chemikali. Inasikitisha kuona watu hasa Dar es Salaam wakifuturu kwa
kutumia soda au juisi ya viwandani zenye utamu sana. Huu utamu unatokana
na chemikali ambayo kiafya ni hatari. Nadhani wasomaji mtakumbuka
zamani kulikuwa na vipakiti ukichangab ya na maji unapata
juisi.
Kimoja unachanganya na maji ndoo moja au jagi moja. Hii pakiti ina
chemikali ambayo ni tamu mara kadhaa ya sukari. Mpaka umeshajifunza
tende na umuhimu wa kutafuta elimu zaidi ya mambo ya vyakula.